Na Paul Kayanda, Mbogwe
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita,wameibuka na kutoa tuhuma dhidi ya Ofisa Ardhi wa Halmashauri hiyo Manase Nkuli wakimtuhumu kushirikiana na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Filbert ambaye hajulikani kama ni Mtumishi wa Idara hiyo lakini anafanya kazi zote za Idara hiyo.
Madiwani hao wamedai kutomtambua mtumishi huyo anayetumika kupima ardhi kwa Wananchi wa Wilaya ya Mbogwe jambo ambalo katika kikao chao cha Baraza wametumia muda mrefu kuhoji uhalali wa mtu huyo kufanya shughuli hizo.
Tuhuma hizo ziliibuliwa kwenye kikao hicho kilichokuwa na lengo la kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ambapo Diwani wa Kata ya Nyakafuru Paul Ngusa alimlalamikia Ofisa Ardhi Nkuli aliyeruhusu kishoka huyo kupima na kabariki ujenzi holela bila kufuata utaratibu wa Mipango Miji na kusababisha Migogoro ya Ardhi katika Kata yake.
“Mheshimiwa mwenyekiti mimi nizungumze eneo la kitongoji cha Shinyanga ‘A’ ni siku chache nimepigiwa simu na wananchi wangu kwenda kujiridhisha sehemu ambayo Maofia Ardhi wamekwenda na kubariki Ujenzi kwenye kiwanja kidogo ambacho hakifai hata kujenga vyumba vitatu vya kuishi mwananchi,” amesema Diwani Ngusa.
Katika kikao hicho Diwani Ngusa pamoja na wenzake waliliomba baraza hilo limtake Ofisa Ardhi huyo aweke bayana majina ya mlalamikiwa huyo pamoja na wadhifa wake katika Idara hiyo ili baraza hilo lijilidhishe kama ni mtumishi halali wa Halmashauri jambo ambalo Ofisa Ardhi huyo hakuweza kuwaweka bayana Madiwani hao.
Baada ya Mjadala mkali uliochukua takribani saa nzima Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Vicent Busiga alionyesha kukerwa na tabia za Ofisa Ardhi huyo kushindwa kuikusanyia Mapato ya Halmashauri ya Mbogwe licha ya kutengewa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya idara hiyo.
“Hili ni baraza la tatu sasa, tunatoa maelekezo Ofisa Ardhi ameshindwa kubainisha kuwa Filbert ni nani ni kibarua ama mtumishi, Sasa hivi tunakupa njia mbadala kwamba kaunde kamati ili uletewe taarifa nadhani ungekuwa unapewa taarifa hili la ujenzi holela lisingeweza kutokea kutokana na kukumbatia haya matokeo yake umeonekana hufai,” amesema Mwenyekiti wa Halmashauri.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa anaungana na madiwani hao kuwa Ofisa Ardhi huyo hatoshi, kulingana na matendo yake iwapo hatabadilika na kutekeleza majukumu yake kwenye idara hiyo.
Akitoa ufafanuzi mbele ya Baraza la Madiwani hao Ofisa Ardhi huyo Manase Nkuli alikili kuwa Wilaya ya Mbogwe inakuwa kwa kasi na kuahidi kufanyia kazi mapungufu yote yaliyotajwa kwenye kikao hicho na kwamba Madiwani hayo wataona mabadiliko kuanzia jumatatu ijayo.


.png)

Post a Comment