Wajane Washauri Wa Kutunza Familia zao

 WANAWAKE waliofiwa na waume zao (Wajane) wametakiwa kutokimbilia kuolewa badala yake waangalie ustawi wa familia kwanza ili kuwapatia watoto wao fursa za elimu na mambo muhimu kwenye maisha.



Hayo yamesemwa na mlezi wa wajane kata ya Nkuhungu  halmashauri ya Jiji la Dodoma Ashura Kimwaga wakati wa mkutano wa wanachama wa chama cha wajane wa kata hiyo.

Kimwaga alisema kuwa wajane wengi wamekuwa wakikimbilia kuoolewa na kuacha watoto wakihangaika huku wengine wakipoteza mali walizoachiwa na wenza wao ambazo zingeisaidia familia.

“Ukifiwa katika umri mdogo unaweza kuolewa, lakini wale wenye umri kama wangu tulia ulee watoto na wajukuu, wengi wamepoteza mali walizokuwa nao kwa sababu ya kuingia kwenye ndoa na mahusiano yasiyo sahihi na kupelekea kile alichoachiwa kwa ajili ya familia kupotea “,” alisema

Aliwataka wanachama wa chama hicho kushikamana ili fedha zitakazopatikana kutokana na michango ya wanachama na wadau wengine kitumike kama mtaji wa kuanzizha miradi ambayo itawakomboa kiuchumi.

Alisema kuwa  chama hicho kilianzishwa Oktoba 2022 kikiwa na wanachama 102 na sasa kuna wanachama 284.

Alisema kuwa changamoto kubwa ni baadhi ya wajane kutokuwa na uwezo wa kulea familia na kusomesha watoto, kudhurumiwa mali zao. Kutengwa, kunyanyaswa.

“Wengine wamejiingiza kwenye mikopo kausha damu, hivyo kupelekea kuchukuliwa vitu vya ndani,” alisema

Alisema kuwa umoja huo unaundwa na mitaa saba ya kata ya Nkuhungu ambayo ni Bochela, Itega, Salala, Mnyakongo,Amani,Muungano na Mtube.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi mkoa wa Dodoma Mary Mabhaya alisema kuwa wanawake hao wataunda vikundi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kisha watapatiwa elimu itakayowawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Alisema kuwa  miradi hiyo itawawezesha kuwa na uhakika wa kipato na hivyo kujiinua kiuchumi wao na familia zao.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) kata ya Nkuhungu, Mahija Mataka aliwataka kutokuwa wachoyo katika kuambiana fursa kwani lengo ni kuinuana kiuchumi

 

Diwani wa Viti Maalum Kata ya Nkuhungu,  Rose Nitwa aliwataka wajane kuendelea kujiamini na kujishughulisha na kazi mbalimbali ili kuweza kuongeza vipato vya familia.

Alisema kuwa wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ambapo wajane ni muongoni mwa wanufaika ili kuwapunguzia magumu ya Maisha.

Alisema kwa siku za hivi karibuni alitoa vyakula, nguo, magodoro na vifaa vya shule kwa familia zenye mahitaji.

 Mwenyekiti wa mtaa wa Bochela , Julius Macheya alisema kuwa ni muhimu kwa wajane kuwa kwenye vikundi hali itakayosaidia kuwapanua mawazo na kuwajenga na kujiinua kiuchumi.

“Usikae peke yako ndani umejifungia unalia, tafuta wenzio make nao mbadilishane mawazo yatakayowajenga na kutafuta mbinu za kujikwamua msiwe wepesi wa kukata tamaa,” alisema

 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Bochela, John Masaka aliwataka wajane hao kuwa na mipango mizuri katika utekelezaji wa shughuli wanazofanya ili ziwe na tija.

“Wengi wanapoachwa wanakuwa hawana cha kufanya,huwa wanakuja hadi serikali za mitaa kuomba msaada lakini ukiangalia hakuna mpango wa kusaidia wajane, lakini sasa wanasaidiwa kupitia wadau na mashirika mbalimbali,” alisema

 Mmoja wa wageni waalikwa katika mkutano huo, Caroline Sanga aliwataka wajane kujiamini, kujipenda na kuweka mbele vipaumbele muhimu kwenye maisha ikiwemo kusomesha watoto.

“Somesheni watoto watawasaidia huko baadaye na hata wao watakuwa na Maisha yenye uhakika, usiangalie huyu ni mtoto wangu au huyu ni mtoto wa mume wangu wapende wote bila kubagua,” alisema

Post a Comment

Previous Post Next Post