Na Paul Kayanda, Nyang’hwale.
KATIBU Mkuu wa Mgodi wa Igalula Gold Mine uliopo Wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita Bw.Makamba Mussa Lameck, akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake juu ya tahadhali za kutokea kwa ajali Migodini amesema kuwa hakuna Mgodi wowote nchini unaofurahishwa na kuwepo kwa ajali.
Januari 13, mwaka huu watu 22 walifariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi cha Udongo(GEMA) wakati wakiendelea na shughuli za Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu kwenye moja ya Migodi Mkoani Simiyu.
Kufuatia hali hiyo Katibu mkuu wa Mgodi wa Igalula Lameck amesema kuwa wao kama mgodi walichukua hatua hiyo mapema kabla ya kuwepo tetesi ya Mvua nyingi za Elinino na kwa kipindi hiki wamejipanga vyema kukabiliana na Mvua hizo.
“Isipokuwa vitu vingine hutokea aidha kwa mipango ya Mungu, mfano kama sisi ajari zinazotokea hapa na ukija kufuatilia pale ukaguzi unapofanyika huwezi kukuta duara duara haijafungwa ni vile duara inakuwa imefungwa vizuri na hiyo kwa hiyo ajali inatokea kwa kuteleza na asilimia kubwa huokolewa wakiwa hai,” amesema Bw.Makamba Mussa Lameck katibu wa Mgodi wa Igalula.
Amesema kuwa kipindi cha nyuma vifo vilitokea kwenye Mgodi wao lakini tangu mwaka jana mwezi wa kumi mpaka sasa hakuna kifo chochote kilichotokea na kuongeza kuwa uongozi wa Mgodi upo Makini ikiwemo kusimamia sheria walizojiwekea lakini zile za Tume ya Madini.
Pia ametumia nafasi hiyo kushukuru Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Mbogwe Jeremia Hango kwa ushirikiano baina yake na wachimbaji kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo usalama wao.
“Tunazidi kuiomba Ofisi ya Madini Mkoa wa Kimadini Mbogwe kuendelea kuwa karibu na sisi wachimbaji lengo ni itukumbushwe wajibu wetu wa kuhakikisha tunachimba Madini hayo katika hali ya Usalama zaidi lakini kuhimiza sheria zilizowekwa na serikali kwa ujumla,” amesema katibu huyo.
Akizungumzia mafanikio ya Kikundi cha Igalula Gold Mine Katibu Mkuu huyo alimpongeza Mkurugenzi wa Mgodi huo Hussein Makubi maarufu Ng’wananyanzala kwa kuwajali wachimbaji na kusikiliza kero zao.
“Kwa kweli mafanikio yanayoonekana na mgodi huu kufanya vizuri inatokana na Mkurugenzi wetu kuwa msikivu, anajali anasikiliza na kutatua kero za watumishi wake haraka lakini anafuata matakwa na masharti ya usimamizi wa leseni za Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu, Amesema Katibu.
Pamoja na mambo menginea Katibu huyo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi shupavu wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuthamini mchango wa Sekta ya Madini na hasa wachimbaji wadogo.

.png)

Post a Comment