307 Wanafuzu Cheti Cha Juu Cha PSPTB

 

Na Mwandishi Wetu 

WATAHINIWA 307 waliofanya mitihani ya awamu ya 27 ya cheti cha juu cha wataalamu wa ununuzi na ugavi (CPSP) wamefuzu, ikiwa ni kati ya watahiniwa 932 waliofanya mitihani hiyo muhimu mwezi Novemba, mwaka jana.

Idadi hiyo  ni sawa na asilimia 32.9 ya watahiniwa wote waliofanya mitihani hiyo inayoratibiwa na Bodi ya Wataalamu wa  Ununuzi na Ugavi (PSPTB).



Akitangaza matokeo hayo yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu jana Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB Bw. Goodfred Mbanyi alisema kuwa jumla ya watahiniwa 20 wamefeli kabisa mitihani hiyo, na kwamba watahiniwa 605 wanatakiwa kurudia baadhi ya masomo ambayo wamepata alama ndogo chini ya viwango vya ufaulu vinavyotakiwa.

"Ni changamoto kwamba takribani watahiniwa 20 watalazimika kurudia mitihani yote kwani wamepata matokeo mabaya kwenye mitihani yao yote," alisema.

Hata hivyo, aliwaasa watahiniwa waliopata matokeo mabaya kuanza kufanya maandalizi mapema ili kurudia mitihani hiyo muhimu itakayofanyika mwezi Mei, mwaka huu.

Amesema, watahiniwa hao bado wana nafasi nzuri na uwezo wa kutosha kufaulu mitihani hiyo endapo watapata muda wa kutosha wa kujiandaa.

Aliyataja masomo ambayo watahiniwa wengi wameshindwa kupata alama zilizopendekezwa za ufaulu kuwa ni pamoja na Basic Commercial Arthmetic, Principle of Book- Keeping, Decision Making Techniques and Project Management.

Alitaja baadhi ya mambo ambayo yamechangia matokeo hafifu miongoni mwa watahiniwa kuwa ni pamoja na maandalizi duni, ukosefu wa mbinu zinazohitajika katika kujibu maswali pamoja na ukosefu wa vituo sahihi vya kupata mafunzo ya taaluma husika.



Bw. Mbanyi alieleza kuwa, uandikishaji kwa watahiniwa wapya wanaotaka kufanya mitihani hiyo muhimu, pamoja na wale wanaotakiwa kurudia upya umepangwa kuanza Januari 22, 2024.

“Mitihani inayofuata itafanyika kuanzia mwezi Mei 13 hadi 17, katika vituo mbalimbali vilivyochaguliwa, vikiwemo The Law School (Dar es Salaam), TIA-Mbeya (Mbeya), Chuo cha Elimu ya Biashara-CBE (Dodoma), SUAT (Mwanza), TRITA (Moshi) na Kituo cha Elimu Mbadala (Zanzibar).

"PSPTB inapenda kuwatia moyo na kuwaelekeza watahiniwa waliopata matokeo duni kujiandaa vyema ili kufanya mitihani hiyo kwa ufaulu, lakini pia tunatoa wito kwa wahitimu wapya kujiandikisha ili kufanya mitihani," Bw Mbayi alieleza. .

Alisema, sekta ya ununuzi na ugavi nchini inakabiliwa na changamoto ya idadi ndogo ya wataalamu wanaohitajika, na kusema Bodi hata hivyo inafanya kazi usiku kucha kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na idara nyingine zinazohusika ili kusaidia kuziba pengo lililopo kwenye sekta hiyomuhimu.



Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa Sheria namba 23 ya mwaka 2007. PSPTB ina majukumu ya kuendeleza, kufuatilia na kudhibiti Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi katika sekta ya umma na binafsi nchini

Post a Comment

Previous Post Next Post