Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWANASIASA nguli nchini, waziri Mkuu mstaafu John Samuel Malecela amesema kuwa, kinyume na nchi nyingine ndani ya bara hili, Tanzania imefanikiwa kupata mafanikio makubwa tangu ilipopata uhuru wake,mwaka 1961.
Mbali na kushuhudia ustawi mkubwa katika upande wa ukomavu wa kisiasa, uhuru wa kujieleza na utawala bora, nchi imeendelea kushuhudia mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi, hali ambayo imechochea kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na maendeleo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, alielezs Mzee Malecela.
Akifanya mahojiano maalum na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru jana nyumbani kwake Jijini Dodoma, alieleza kuwa nchi nyingi barani Afrika ambazo zilipata uhuru katika kipindi kimoja na Tanzania zimepitia machafuko makubwa ya kisiasa, na kuyumba kiuchumi, kinyume na Tanzania.
“Pamoja na changamoto kadhaa, leo hii Tanzania inasimama miongoni mwa nchi ambazo ukuaji wa uchumi wake kwa mwaka ni wa kuridhisha, lakini pia nchi imeweza kupiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma muhimu za kijamii,” alisema.
Kwa mfano, alieleza kuwa Serikali ya awamu ya sita hadi sasa imefanya kazi na imeweza kuhakikisha usambazaji na upatikanaji wa maji salama kutoka mijini hadi vijijini pamoja na huduma za umeme, afya na elimu.
"Ni mafanikio makubwa ya kiuchumi kwamba serikali kwa sasa inakamilisha kazi ya ujenzi wa mradi wa Bwawa la Umeme wa Maji la Julius Nyerere, kituo chenye thamani ya trn 6.55/- ambacho kimefadhiliwa kwa asilimia 100 na serikali," alisema.
Aidha, mzee Malecela alieleza kuwa, mbali na kukidhi mahitaji ya ndani ya umeme, hatua ambayo inatarajia kuchochea kasi ya uchumi wa viwanda, kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha nchi kuuza umeme kwa nchi mbalimbali jirani.
Akizungumza juu ya utawala bora na maadili kwa viongozi wa umma, Malecela amesema Serikali inafanya vizuri katika kusimamia sekta hiyo, japonica bado kuna viongozi wachache wa umma ambao hawana moyo wa kizalendo na maadili katika utendaji kazi wao.
“Inafurahisha sana kuona namna Rais Dk Samia Suluhu Hassan anavyofanya kazi ya kukuza demokrasia nchini, ni kiongozi mzuri anayetekeleza vyema demokrasia ya uwakilishi, ataiongoza nchi kwenye maendeleo yanayosubiriwa kwa hamu,” aliongeza. .
Aliongeza kuwa, akiwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia anatoa mchango mkubwa wa kukuza ukomavu wa kisiasa ndani ya chama hicho tawala, hatua inayoshuhudia chama hicho kikitimiza Ilani zote za chama hicho.
"Wakati tunasherehekea miaka 62 ya Uhuru wetu leo, wito wangu kwa Watanzania wote ni kwamba, tunapaswa kusimama pamoja katika kumuunga mkono Rais Samia kutafsiri katika uhalisia dira yake nzuri ya maendeleo ya kiuchumi.
"Huu siyo muda wa kuwekeana chuki za kisiasa, bali ni wakati muafaka wa kufanya 'siasa safi' kwa ajili ya maslahi mapana ya kuchochea kasi ya maendeleo," alisisitiza waziri mkuu huyo wa zamani.
Malecela alizaliwa mnamo tarehe 19 Aprili, mwezi Aprili 1934 katika eneo la Bugiri Dodoma na alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Novemba 1990 hadi Desemba 1994.

Post a Comment