Samia azitaka nchi za EAC kutotegemea wahisani kwenye majanga ya mabadiliko ya tabia nchi


RAIS Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutotegemea wahisani kutoka ughaibuni kama misaada ya kupambana na majanga yatokanayo  na mabadiliko ya hewa 


Alisema bara la Afrika ni mama wa mazingira hivyo nchi za EAC zisikubali tena kuharibu mazingira kwa kutegemea misaada ya kifedha kutoka nchi.


RAIS alisema hayo jana kwenye Mkutano wa ngazi ya juu wa 23  wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha wakati akiwahutubia viongozi mbalimbali wakiwemo marais watatu na wawakilishi wa marais 3 wa EAC


"Tusiwategemee wengine kuja kutupa fedha za majanga ya mabadiliko ya hali ya hewa.Nashauri huu uwe ujumbe wetu kwa nchi za EAC kwenye mkutano ujao wa dunia wa COP28 kuhusu mazingira" alisema


Alisema bara la Afrika bado lina mazingira mazuri  sana na kuna fursa hivyo mataifa ya nje wanapenda kuja kutumia rasilimali  hivyo nchi za EAC zinatakiwa kuanza kutumia mapato yake kwenye majanga ya tabianchi


"Wenzetu huko wameishaharibu hawana mazingira  tena. Tunatakiwa kulinda mazingira yetu, hivyo tukatae masharti. Haiwezekani sisi tunalinda halafu makampuni ya nje yanakuja kuvuna" alisema


Rais pia alizitaja  juhudi mbalimbali zinazofanywa na  serikali katika kukabiliana na majanga ya mabadiliko ya tabia nchi


Baadhi ya  juhudi hizo ni pamoja na serikali kuondoa kodi kwenye pembejeo za kilimo kwa ajili ya kukuza kilimo na usalama wa chakula, kuondoa ushuru na vivutio vyote vya kodi kwenye bidhaa zinazotumika kuzalisha nishati mbadala kwa ajili ya kulinda mazingira.


"Sasa hivi tunahamasisha sekta binafsi kuchangamkia fursa zinazotokana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuanzisha vituo vya utafiti nchi nzima. Hapa tunataka sekta binafsi washiriki kwa kuongeza thamani bidhaa za mazao ya kilimo" alisema

Kwa Upande wake  Mwenyekiti anayemaliza muda wa EAC RAIS wa Jamhuri ya Burundi Evariste Ndayishimiye alisema dunia iko kwenye matatizo makubwa ya ukame na mafuriko hivyo nchi za EAC lazima zinatakiwa kwa pamoja kuja upya na sera mpya zitakazozinusuru kutoka kwenye janga la mabadiliko ya tabia nchi.


"Tunahitaji kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dni na wadau wengine wa maendeleo" alisema


Alisema mahitaji makubwa kwa nchi za EAC ni kuwa na teknolojia, uafiti wa kina na uwekezaji katika masuala ya mazingira


"Ili kuwa na usalama wa chakula lazima tuwekeze kwenye utafiti na teknolojia na tunahitaji sera ya kanda kuhusu mabadiliko ya tabia nchi" alisema



Mkutano wa wakuu wa nchi unahirishwa leo kwa Rais wa Ndayishimiye kukabidhi kijiti kwa Rais Salva Kiir wa Jamhuri ya Sudan   Kusini. Katika mkutano huu Marais Paul Kagame (Rwanda), Yoweri MUSEVENI (Uganda), Felix Tshekedi ((DR Congo) wametuma wawakilishi



Post a Comment

Previous Post Next Post