Polisi Mwanza Kukagua Nyaraka Muhimu Kampuni Binafsi za Ulinzi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza leo Novemba 20, 2023 limeendelea na ukaguzi wa kampuni binafsi za ulinzi katika Wilaya ya Ilemela ambapo Kampuni ya West Security Services, Intelligence Securico na Masa Security Services Limited zimefanyiwa ukaguzi.


Zoezi hilo limeongozwa na Afisa Polisi Jamii Mkoa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhani Sarige akiwa ameambatana na Mrakibu wa Polisi (SP) Denis Rwiza, mkaguzi wa Polisi (Insp) Jovitha Tibangayuka na mkaguzi msaidizi wa Polisi (A/Insp) Emmanuel Mwakalindile (Mkaguzi wa Kata ya Nyamanoro).

Wakati wa ukaguzi huo, ACP Sarige amebaini baadhi ya mapungufu ikiwemo walinzi kutokuwa na sifa za kufanya kazi ya ulinzi na wamiliki wa kampuni kutopeleka makato ya michango ya watumishi wao kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Kupitia zoezi hilo, ACP Sarige amewataka Wakuu wa Polisi wa Wilaya pamoja na Wakaguzi Kata kufanya ukaguzi wa kina kwa kuangalia nyaraka muhimu zinazotakiwa kuwepo kwenye kampuni binafsi za ulinzi na vitendea kazi vingine kwa mujibu wa sheria.




Aidha, ACP Sarige amewataka Wakurugenzi na Wamiliki wa kampuni zote za ulinzi kutoa ushirikiano na kuwasilisha nyaraka muhimu wakati wa ukaguzi huo.





Post a Comment

Previous Post Next Post