Mavunde Asimamisha Leseni za Uchimbaji Madini Za Kampuni Ya ADOYOO

 Na Paul Kayanda, Kahama


 


WAZIRI wa Madini Antony Mavunde amesimamisha Leseni zote za Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu za kampuni ya Adoyoo Minerals iliyotakapaa nchi nzima baada ya kukamatwa wakati akijaribu kutorosha Dhahabu Kilo 4.3 zenye thamani ya Shilingi Milioni 562,288,207.

 

Octoba 11 mwaka huu majira ya saa tatu usiku Waziri Mavunde alitembelea Soko la Dhahabu Kahama  na kukutana na wafanyabiashara wa Dhahabu ambapo alidai amesikitishwa na kitendo cha utoroshwaji wa Madini hayo na kuwatamkia kuwa hatavumilia vitendo hivyo.



 

Kufuatia hali hiyo Waziri mavunde alisema kuwa atamwagiza katibu mtendaji Yahaya Samamba ili asimamishe leseni zote nchi nzima za kampuni ya Nadoyoo Minerals Trading baada ya kukamatwa mmoja wa wahusika wa kampuni hiyo akijaribu kutorosha  Madini ya Dhahabu Dhahabu kilo 4.3 yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 500.

 

“Serikali ya awamu ya sita chini ya mama yetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan haitakubali kuona watu wachache wanajihusisha na suala la utoroshaji wa madini, nataka niwaambie tu tutachukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayekamatwa anatorosha madini hayo, mimi nimefurahi kuona vijana wadogo mnafanya biashara hizi ila angalieni msije mkapotea fanyeni biashara halali,” alisema Antony Mavunde Waziri wa Madini.

 

“Mimi nina mwezi mmoja tu nikiwa Wizarani, nimekuwa nikiongoza wachimbaji kupitia FEMATA sasa wachimbaji msiseme nitawahurumia, na kuanzia leo, mtu yeyote atakayekamatwa kwa kosa la utoroshaji madini ajue chamoto atakiona,” alisema Mavunde na kuongeza.

 

“Kwa mana hiyo aliyebainika sasa tutakwenda kusimamisha leseni zake zote nchi nzima wakati tukisubili hukumu ya vyombo vya sheria na iwapo atabainika mhusika anahatia tutachukua hatua kali ikiwemo kufuta leseni zote na kuhakikisha kuwa mhusika hatajihusisha na Uchimbaji wala biashara ya madini katika maeneo yote nchini,” alisema.

 

Pia Mavunde alisema kuwa pamoja na hatua kali za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya watoroshaji hao pia madini yote yatakayokamatwa yatahifadhiwa na serikali na kupelekwa Benki kuu ya Tanzania(BOT)  kusubili hatima ya Mahakama.

 

Naye afisa Madini mkazi wa Mkoa wa Kimadini Kahama Jeremia Hango aliwaambia waandishi wa habari kuwa Tukio la mfanyabiashara huyo kutaka kujaribu kutorosha Dhahabu lilitokea Oktoba 10 kuanzia majira ya saa 1 hadi saa 4 usiku huko Nyumbani kwake Nitesh katika Mtaa wa Nyasubi manispaa ya Kahama Mkoani hapa.

 

Aidha  afisa Madini huyo alibainisha kuwa mtuhumiwa huyo angefanikiwa kutorosha Dhahabu hizo alikuwa anaikosesha serikali Milioni 150 za Mrabaha, ada ya ukaguzi, ushuru wa huduma pamoja na kodi ya mapato.

 

Akizungumzia kuhusu biashara ya Madini kwenye masoko ya Kahama  Hango alimweleza waziri kuwa jumla ya kilo 562.3 za Dhahabu  zenye thamani ya shilingi Bilioni 74.8 ziliuzwa katika vituo vya madini kwa kipindi cha Julai 1,2023 hadi 10 Octoba 2023.

 

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita alipongeza kazi nzuri inayofanywa na wizara ya Madini kupitia tume ya madini na kutumia mwanya huo kuahidi kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya itahakikisha inaendelea kutoa ushirikiano wa kulinda na kudhibiti na kukomesha suala la utoroshaji wa Madini.

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa wafanyabiashara katika Soko la Dhahabu Kahama, Emmanuel Kidenya alionesha kusikitishwa na kitendo hicho cha baadhi ya wafanyabiashara wa madini hayo kuwa siyo waaminifu na uzalendo.

 

Alisema kitendo hicho kinawafanya wafanyabiashara wasiaminike tena katika jamii na serikali kwa ujumla na kutumia nafasi hiyo kuwaomba wafanyabiashara hao kuwa waaminifu ili kujijengea uaminifu na kuongeza kuwa watafanya vikao vya mara kwa mara kukumbushana namna ya kudhibiti utoroshaji wa madini ya Dhahabu kwani serikali pamoja na wafanyabiashara wenyewe wanapata hasara.

Post a Comment

Previous Post Next Post