Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito
kwa Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha Maisha pamoja na kuinua uchumi wa
Taifa.
Makamu
wa Rais amesema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika Misa Maalum ya Kitaifa ya Kumuombea Baba wa Taifa
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki
Parokia ya Roho Mtakatifu – Babati mkoani Manyara. Amewasihi viongozi na watanzania
kwa ujumla kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuishi katika misingi ya kukemea rushwa,
kupiga vita umasikini, kutojilimbikizia mali pamoja na kukemea matendo mabaya.
Makamu
wa Rais amesema ni wajibu kwa watanzania kumuenzi kwa kuishi maisha aliyoishi Baba
wa Taifa kwa kuwa alitumia elimu na vipaji vyake kwa faida ya wote, alithamini
dhamana aliyopewa, alikuwa mnyenyekevu na mwenye kujisahihisha alipokosea.
Ameongeza kwamba alikemea matendo mabaya yaliochochea mmomonyoko wa maadili,
alikuwa mwanamazingira hodari na alipiga vita umasikini.
Aidha
Makamu wa Rais amelishukuru Kanisa pamoja na taasisi zingine za kidini kwa
ushirikiano wake na Serikali kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile
elimu, afya, mazingira na mengineyo. Amesema serikali itaendelea kushirikiana
vema na kanisa katoliki pamoja na madhehebu yote ya dini katika kuwatumikia
watanzania. Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini kuendelea
kuliombea taifa amani na utulivu.
Misa
Maalum ya Kitaifa ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu Anthony Lagwen na
kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia
Suluhu Hassan, Viongozi mbalimbali pamoja na waumini kutoka maeneo mbalimbali
nchini.




Post a Comment