Haki itendeke kwenye Uchaguzi Wa Mwaka-Mchungaji Dkt.Vangast

 Anna George, DODOMA


MCHUNGAJI kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG URCC) jijini Dodoma,Dkt. Salum Vangast amezitaka mamlaka zote nchini kuhakikisha zinasimamia haki katika uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika mwakani.



Vangast, alitoa wito huo jana wakati akizungumza na waandishi wa mara baada ya kumalizika kwa ibada maalumu iliyoambatana na maombi kwa ajili ya kujiweka wakfu kwa watumishi wa Mungu iliyofanyika kanisani hapo ikiongozwa na Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Dk. Magnus Muhiche.


Mchungaji huyo, alisema Kanisa limefanya maombi kwa ajili ya kujiweka wakfu na kutenbea upya katika uwepo wa Mungu kwa lengo kubwa la kuliombea taifa pamoja na mataifa mengine ili kurejesha hali ya amani na utulivu pale ambapo inaonekana kupotea.



Alisema kuwa ili amani iwepo na utulivu ni lazima watu wawe na hofu ya Mungu na kutambua umuhimu wa kutenda haki.


Aidha, alisema binadamu bila kuwa na Mungu hana tofauti na mnyama hivyo kama watu hawatakuwa na hofu ya Mungu watafanya mambo ambayo ni ya hovyo.


Alisema kila mtu hana buni kwa nafasi yake kutambua umuhimu na thamani ya haki kwakuwa hata vitabu vitakatifu vinaeleza kuwa haki huliinua taifa.


“Kutokana na hali hiyo vyombo vya dola nchini vinatakiwa kuhakikisha vinasimamia haki, amani na utulivu na kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa 2025 haki inatakiwa kutawala na atakayekuwa ameshinda atangazwe kwa ushindi wake na atakayeshindwa atangazwe kwa kushindwa kwake na si vinginevyo”alisema


Akizungumzia kuhusu waumini kushiriki katika uchaguzi alisema ni haki yao na ndiyo maana kanisa linafanya maombi kwa ajili ya taifa kuwa na viongozi wenye hofu ya Mungu.



“Taifa linatakiwa kuongozwa na watu ambao si wabinafsi au wenye chuki na visasi bali wawe watu ambao wamepatikana kihalali na wenye kuhakikisha wanalinda amani ya nchi kwa kuzingatia misingi ya haki na upendo”alisema


 

Post a Comment

Previous Post Next Post