Na Valentine Oforo, Pemba
UMOJA wa Ulaya (EU) kupitia Programu ya Kuwezesha Mnyororo wa Thamani wa Ufugaji Nyuki (Beekeeping Value Chain Support -BEVAC) umekabidhi pikipiki tano kwa Maafisa wa Misitu wa Wilaya za Pemba.
Pikipiki hizo za kisasa zenye thamai ya Shilingi Milioni 43 zimetolewa kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa shughuli za sekta ya nyuki katika Wilaya ya Pemba, Visiwani Zanzibar.
Na Pikipiki hizo zimekabidhiwa kwa wanufaika walemgwa kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo katika hafla maalumu iliyofanyika viwanja vya Maonesho vya Chamanangwe Pemba.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa pikipiki hizo, Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Bw Makame Kitwana Makame amesema pikipiki hizo zitatoa mchango chanya katika kuendeleza utekelezaji wa kazi za kuboresha mnyororo wa thamani katika Sekta ya Ufugaji Nyuki katika kisiwa cha Pemba.
“Pamoja na mambo mengine, vyombo hivi vya usafiri vilivyotolewa leo vitachochea na kurahisisha upatikanaji wa huduma za ugani kwa wafugaji wetu wote waliopo katika kisiwa chetu cha Pemba” alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya BEVAC Pemba, Juma Omari Abdalla amewataka Maafisa wa Misitu waliyopewa pikipiki hizo kuhakikisha wanazitunza vizuri na kuzitumia kwa malengo husika ili kuchochea kasi ya maendeleo ya sekta ya nyuki katika Wilaya hiyo.
Programu ya BEVAC inalenga kuimarisha mnyororo mzima wa thamani ya ufugaji nyuki kwa nia ya kukuza mchango wa sekta katika kuongeza ajira, mapato na usalama wa chakula nchini Tanzania.
Sekta ya ufugaji nyuki nchini inajumuisha mfumo mzima wa usimamizi, utengenezaji na uandaaji wa vifaa mbalimbali, ufugaji nyuki, uvunaji wa asali na mazao mengine, utayarishaji, ufungashaji na uuzaji wa mazao ya nyuki.
Kwa Tanzania, sekta hii inakadiriwa kushirikisha takribani watu zaidi ya milioni 2 hali inayoonesha umuhimu wake mkubwa hasa katika kuongeza kipato kwa jamii.
Sekta imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki (beekeeping value chain) kuanzia uzalishaji, usindikaji na uuzaji wa bidhaa za nyuki hadi mwishoni mwa mfumo mzima unaojumuisha wahusika mbalimbali wanaounganishwa na mtiririko wa bidhaa, fedha, taarifa na huduma.
Katika kutatua changamoto hizo, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, mnamo tarehe 17 Septemba, 2020 ilisaini mkataba wa ufadhili (Financing Agreement-Nam. TZ/FED/040-900) na Tume ya Ulaya (European Commission-EU).
Mkataba huu ni makubaliano ya EU kutoa fedha kiasi cha Euro milioni 10 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa nyuki kwa kipindi cha miaka sita (6) katika mikoa ya Katavi, Singida, Tabora, Shinyanga, Kigoma, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.
Mradi huu ni wa kuwezesha utekelezaji wa Programu ya Kuwezesha Mnyororo wa Thamani wa Ufugaji Nyuki (Beekeeping Value Chain Support Programme-BEVAC).
Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa jukumu la kuratibu shughuli zote za mradi kwa niaba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Katika utekelezaji wa Programu Shirika la Maendeleo la Ubeligiji (ENABEL) ) kwa ushirikiano na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC), limepewa jukumu la kusimamia na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa niaba ya EU.
Kwa upande wa Pemba, Mradi unatekelezwa katika wilaya zote nne za Pemba, yaani Chakechake, Wete, Mkoani na Micheweni.




Post a Comment