ATCL Yajipanga Kuanza Kusafirisha Mazao Ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo Nje Ya Nchi

 Na Agnes Benedict,Morogoro


SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL) limeweka mikakati wa kusafirisha mazao ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo nje ya nchi hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango hivi karibuni wakati wa mapokezi ya Ndege mpya B737 Maxi 9-1.



Akizungumza katika kikao cha tano cha baraza la pili la wafanyakazi kilichofanyika mjini Morogoro Mkurugenzi Mkuu wa ATCL,Ladislaus Matindi amesema kuwa mazao hayo ni pamoja na Parachichi ambalo limepata soko kubwa nje ya nchi yanasafirishwa kwa kutumia Ndege ya mizigo iliyonunuliwa na Serikali.



Amesema tayari Shirika limeanza mazungumzo na wafanyabiashara , wadau pamoja na wakulima jinsi ya kusafirisha bidhaa hizo kwa tija zaidi.



Amesema tunaelekea kwenye msimu wa kilimo ,itakapofika hasa wa zao la Parachichi ambao tumekuwa maarufu sana sisi Tanzania kwa hapa Duniani, tutahakikisha tunalipeleka kwenye masoko ya nje kwa haraka kwa sababu ni zao linaloharibika kwa haraka.


Ametaja mazao mengine yaliyowekewa mkakati wa kusafirishwa kwa haraka kwenda masoko ya nje ni Samaki, Nyama na Maua ambayo yamekuwa yakiharibika kwa haraka.


“ Kitu pekee kinachohakikisha mazao haya yanafika kwa ubora kama ulivyo ni usafiri wa anga ,na tunategemea kuongezeka kwa mazao haya na yatasafirishwa kwa haraka” alisema Mhandisi Matindi


Anasema kuwa kwa upande wa utekelezaji wa mpango mkakati wa pili wa miaka mitano kuanzia 2022/23- 2026/27 ,ni pamoja na kupanua zaidi huduma za Shirika kwa kuongeza miruko kwenye baadhi ya safari.


Hata hivyo Mhandisi Matindi amesema , ATCL inatarajia kuanzisha safari katika maeneo mapya ya Pemba, Tanga, Mafia, Nachingwea na Musoma kwa safari za ndani ya nchi.


Kwa safari za nje ya nchi alizitaja ni Kinshasa, Goma, Dubai, Muscat na Lagos ambapo pia ATCL ikifanikiwa kuongeza vituo kutoka vinne vya ndani na kimoja cha nje ya nchi hadi kufikia vituo 15 vya ndani na vituo 11 vya nje ya nchi.



Akifungua Baraza hilo la Wafanyakazi wa ATCL, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Lucas Kambelenje alilipongeza shirika hilo kwa kuongeza umiliki wa soko la ndani kutoka asilimia 24 mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia asilimia 53 kwa mwaka 2022/23.


Katibu Mkuu wa wizara hiyo pia aliipongeza kwa kufanikiwa kutunza na kuimarisha viwango vya kimataifa katika uendeshaji wa shughuli za usafiri wa anga na kuingia mikataba ya ushirikiano wa kibiashara na mashirika makubwa ya ndege duniani.



Aliyataja mashirika makubwa hayo ni pamoja na Qatar, Emirates, KLM, Air India ,Ethiopia na Oman air ambayo yamekuwa muhimu katika upatikanaji wa abiria ambao unganisha safari kwenda katika maeneo ambayo ATCL haifiki.

Post a Comment

Previous Post Next Post