Na Paul Mabeja, DODOMA
CHAMA cha wazazi wa watoto wenye shida ya kichwa kikubwa na mgogo wazi nchini, kimeiomba serikali pamoja na wadau wengine kusaidia akinamama waliotelezwa na waume zao kutokana na kuzaa watoto wenye tatizo hilo.
Mkurugenzi wa chama hicho Suma Mwaipopo, alisema hayo jana jijini hapa,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kero mbalimbali zinazo wakabili wazazi pamoja na watoto wenye tatizo nchini.
Alisema, asilimia 25 ya akinamama wa watoto wenye tatizo hilo wametelekezwa na wanaume wao hali ambayo inachangia wengi kuwa na maisha magumu na kushindwa kuhudumia watoto hao.
“Wazazi ambao wanaishi na watoto wenye shida hii kwa kiasi kikubwa na wanawake ambao pia wengi wao wametelekezwa na waume zao mara baada ya kuzaa watoto wenye tatizo hili hivyo kusababisha kupitia maisha magumu na kushindwa kumudu gharama za matibabu”alisema Mwaipopo
Alisema, kutokana na hali hiyo wanaiomba serikali pamoja na wadau wengine kukiwezesha chama hicho ili kiweze kusaidia watoto hao kupata matibabu ambayo ni mzigo mkubwa kwa wazazi hivi sasa kuzimudu.
“Matibu kwa watoto hawa ni gharama sana na wazazi wengi wenye watoto hawa maisha yao ni duni kutokana na kutelekezwa na waume zao hivyo kama chama chetu kitawezesha kitakuwa na uwezo wa kuwahudumia kwenye matibabu.
“Matibabu hivi sasa kwa watoto hawa wanayapatia katika hospitali ya Moyi ambapo wanalazimika kukaa kwa takribani wiki moja lakini pia wataambiwa warudi tena hivyo gharama kwao ni changamoto kubwa sana”alisema
Kadhalika, alisema katika kukabilina na hali hiyo chama hicho kimefanya jitihada mbalimbali za kusaidia wazazi na watoto wenye shida hiyo ambapo hadi sasa watoto 12,000 wamepatiwa misaada mbalimbali.
Pia, alisema chama hicho kimejenga nyumba jiji Dar es Saalam ambayo inatumia kama nyumba ya matumaini kwa ajili ya kuhuduma wazazi wanaotoka mikoa mbalimbali wanaokwenda kusubiri huduma za matibabu.
“Chama chetu hivi sasa kinafanya kazi katika mikoa 11 na kinawachama 7,000 lengo letu ni kusaidia watoto hawa kwa kuwapatia matibabu ikiwemo kutoa bima za afya lakini pia nyumba hii inapunguzia gharama.
“Tatizo hili na kichwa kikubwa na mgogo wazi wataalam wanasema linatokana na upungufu wa madini ya foric acid kwahiyo tunaelimisha jamii ili kupunguza tatizo hilo na kuzaliwa kwa watoto wenye shida hii”alisema
Aidha, alisema lengo la chama hicho ni kuhudumia watoto 1,500 kila mwaka mwenye shida hiyo lakini kutokana na ufinyu wa bajeti mwaka jana wamehudumia watoto 1,230.



Post a Comment