Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan hapa nchini, Mhe. Yasushi Misawa katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Septemba 14, 2023 Dkt. Jafo amemshukuru Balozi Misawa kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo (JICA) kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji, elimu, barabara, afya na kuiomba Serikali hiyo kusaidia pia miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira iliyopo nchini.
Waziri Jafo amemueleza Balozi Misawa kuwa ajenda ya
mazingira ni moja ya kipaumbele muhimu vilivyopewa msukumo na Serikali ya Awamu
ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Serikali kupitia
Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea na juhudi za kuhamasisha jamii kutumia
nishati mbadala ili kuhamasisha uhifadhi na utunzaji mazingira nchini.
“Tanzania tunazalisha takribani tani Milioni moja za taka ngumu ambazo ni fursa ya uzalishaji wa nishati mbadala…tunatumia asilimia 30 tu ya nishati hiyo…Tunahitaji nishati hii kwa ajili ya matumizi ya kijamii na kiuchumi. Tunahitaji wawekezaji wengi zaidi kujitokeza kwa ajili ya uwekezaji,” amesema Mhe. Dkt.Jafo.
Amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki
kwa wawekezaji na wadau wa nishati hiyo kuweza kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati mbadala hususani katika maeneo ya vijijini ili kuongeza
upatikanaji wa nishati mbadala ya kupikia.
Waziri Jafo pia amemhakikishia Balozi Misawa
ushirikiano na utayari wa Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha utekelezaji
wa miradi ya nishati jadidifu
ikiwemo jotoardhi, tungamotaka, upepo na jua pamoja na matumizi bora ya Nishati mbadala ili kuleta manufaa
kwa wananchi na jamii kwa ujumla.
Akifafanua zaidi Waziri Jafo amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa sera, kanuni na miongozo mbalimbali ikiwemo ikiwemo katazo Kwa taasisi zote za umma na binafsi kwa upande wa Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi 300 kusitisha matumizi ya mkaa na mkaa ifikapo mwaka Januari 2025.
Post a Comment