NEMC Yawataka Wamiliki Wa Mabasi Nchini Kuzingatia Utunzaji Wa Mazingira



Na Mwandishi Wetu,  Dar es Salaam 

BARAZA  la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wamiliki wa mabasi kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kuweka vyoo na vitenganishi taka kwenye mabasi yao wanapokuwa safarini.
 Agizo hilo limetolewa na  Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Mafwenga Gwamaka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na abiria kwenye mabasi pamoja na namna sahihi ya kudhibiti uchafuzi huo.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa NEMC Jijini Dar es Salaam,  Mkurugenzi huyo mesema abiria wa mabasi wamekuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira kwa kutupa taka madirishani na kuchimba dawa maporini  wakati wa safari ndefu, hali inayopelekea kuhatarisha maisha yao pamoja na kuchafua mazingira, hasa vyanzo vya maji.

"Kumekuwa na tabia ya abiria kutupa mabaki ya vyakula madirishani popote pale, au kwenda haja kubwa na ndogo wakati wa safari ndefu barabarani, ikiwa ni pamoja na maeneo ya hifadhi za misitu na  mbuga za wanyama," alisema.

Aidha, amesema, maeneo ya hifadhi na barabara zote zinatakiwa kulindwa, na hivyo sio nzuri i kuchafua mazingira ya maeneo hayo muhimu ya nchi.

Ameongeza kuwa mabasi yote ya abiria yanayofanya safari ndefu yanapaswa kuzingatia kanuni za utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kuweka vitenganishi vya taka kwenye mabasi, hali itakayosaidia kuepuka uchafuzi wa mazingira.

Dkt. Gwamaka amesisitiza kuwa uchafuzi aina hii una athari kubwa katika mazingira kwani huibua magonjwa ya mlipuko, husababisha kuchafuliwa na kuziba kwa  vyanzo vya maji, na pia  hupelekea mikondo ya maji kuziba, kusababisha mchafuko wa hali ya hewa pamoja na kuharibu ikolojia ya wanyama na mimea.

Amezitaka Halmashauri kote nchini kwa kushirikiana na Chama Cha Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji ( TABOA) pamoja na LATRA kuhakikisha elimu ya utunzaji wa mazingira inatolewa na kujenga vyoo maeneo husika ili kuepukana na adha hiyo ya uchafuzi wa mazingira.

Katika hatua nyingine, Dkt. Gwamaka amewataka wenye viwanda kuhakikisha wanazingatia mpango wa kutunza mazingira kwenye maeneo yao ya kazi kwa kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kuhifadhi taka za viwandani na majumbani ili kutunza Mazingira.

Vilivile ameitaka jamii kuwa na tabia ya kutenganisha taka za plastiki, kielekroniki, chuma, karatatasi na mabaki ya vyakula kuanzia majumbani ili kupunguza mzigo kwa Halmashauri wa ukusanyaji wa taka sababu taka ni fursa zinarejerezwa na kutoa ajira pamoja na  malighafi nyingine za viwandani.


Post a Comment

Previous Post Next Post